Wednesday, June 23, 2010

KENYA imeanza kusajili namba zote za simu

NAIROBI,Kenya

KENYA imeanza kusajili namba zote za simu za mkononi kwa nia ya kupunguza uhalifu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini humo, watumiaji wa simu watatakiwa kuonesha vitambulisho na ushahidi wa anuani ya mahala wanapoishi.

Serikali inasema, namba yeyote itakayokuwa haijsajiliwa ifikapo mwisho wa mwezi Julai mwaka huu itafungwa.


Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC,Bw. Odhiambo Joseph aliripoti kutoka mjini Nairobi akisema kuwa watu wengi wameonekana kuunga mkono hatua hiyo, wakiwa na matumaini ya kupunguza uhalifu.

Alisema, magenge ya watekaji nyara wamekuwa wakitumia namba zisizosajiliwa kudai ongo.

Kamishna wa Polisi,Bw. Mathew Iteere aliiambia BBC kuwa simu za mkononi lazima zisajiliwe kwani siku hizi zina uwezo wa kutumika kama kompyuta.

"Imekuwa chombo cha benki, inaweza kutumika kuiba taarifa, kutuma maelezo yasiyoruhusiwa na makosa ya udanganyifu."alisema kamanda huyo.

Wiki iliyopita ofisa katika Wizara ya Habari,Bw. Bitange Ndemo alisema kusajili namba hizo kutasaidia mamlaka husika kupambana na ugaidi, biashara haramu ya dawa za kulevya, pamoja na kujua wanaotuma ujumbe wenye chuki.

Nchi jirani ya Tanzania imeshaanza kutumia mfumo huo na mwandishi huyo wa BBC anasema haina utata wowote.

Alisema eneo aliloenda kulitembelea lilikuwa limejaa watu waliokuwa wakisajili namba zao.

Kenya ina takriban watumiaji milioni 20 wa simu za mkononi na karibu nusu ya idadi ya raia wote nchini humo wana mfumo mzuri sana wa huduma za benki kupitia simu za mkononi.(BBC)

No comments:

Post a Comment