Friday, August 9, 2013

MBUNGE ADAI KUJUA KIINI CHA MOTO UWANJA WA NDEGE


 
Irshad Sumra
Mbunge wa Embakasi Kusini Irshad Sumra. Picha/MAKTABA 
Na MWANDISHI WETU
Imepakiwa - Thursday, August 8  2013 at  11:20
Kwa Mukhtasari
Mbunge wa Embakasi Kusini Irshad Sumra amedai kuwa ana habari kuwa mkasa wa moto wa jana  katika uwanja wa JKIA ulisababishwa na hitilafu za nguvu za umeme uliotokana na ubomoaji wa maduka ya Duty Free.

MBUNGE wa Embakasi Kusini Irshad Sumra Jumatano alidai kuwa alikuwa na habari kuwa mkasa huo wa moto wa Jumatano katika uwanja wa kimataifa  wa Jomo Kenyatta uliosababishwa na hitilafu za nguvu za umeme uliotokana na uvamizi uliofanyiwa maduka ya Duty Free.
“Nimepata habari kwamba vijana 350 waliotumwa juzi kuwafurusha waliokuwa wamiliki wa maduka ya Duty Free ndio walivuruga nyaya za stima ambazo husambaza umeme hadi katika eneo la hili la mkasa,” akasema Bw Sumra.
Mwanasiasa huyo alisema operesheni hiyo iliyofanywa usiku haikusimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) wala maafisa wa Halamashauri ya Safari za Ndege Nchini. Alieleza kuwa  ufurushwaji huo uliendeshwa bila kuzingatia tahadhari zozote za kiusalama.
“Je hao vijana waliotumwa kuwafurusha watumishi wa Duty Free walisimamiwa na nani? Na je, mbona walitekeleza operesheni hiyo usiku?” akauliza Bw Sumra ambaye ni Mbunge wa chama cha ODM.
Alisema kuwa yuko tayari kutoa habari hizo kwa Kamati iliyoteuliwa kuchunguza chanzo cha mkasa huo ambao ulikwamisha hudumu zote katika uwanja huo wenye shughuli nyingi zaidi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. Kamati hiyo ambayo ilianza kufanya kazi mara moja iko chini ya uenyekiti wa Waziri wa Uchukuzi na Miundo Mbinu Mhandishi Michael Kamau.
“Niko tayari kutoa maelezo haya mbele ya kamati hiyo ya kwani naamini yatasaidia katika kutanzua chanzo cha tukio hili la kusikitisha. Hata jana sisi kama wabunge tulijadili suala hili la ufurushaji wa wamiliki wa Duty Free katika Bunge,” akawaambia wanahabari huku akilalama kuwa hakushirikishwa kwenye kamati hiyo.
Mita 50
Hata hivyo waziri Kamau alipuuzilia mbali madai hayo akisema kuwa maduka hayo yako umbali wa mita 50 kutoka eneo la mkasa.
“Moto huu ulitokeo katika eneo la huduma za uhamiaji ndipo ukasambaa kote. Hauhusiani kwa vyovyote na ufurashaji uliofanyika katika Duty Free,” akasema huku akiomba wadau wote wasubiri uchunguzi kamili.

No comments:

Post a Comment