MWANAMUME AJINYONGA BAADA YA RAILA KUPOTEZA KESI
Na ELISHA OTIENO
Imepakiwa - Monday, April 1 2013 at 17:37
Kwa Mukhtasari
Mwanamume anayedaiwa kuwa mfuasi sugu wa ODM alijinyonga katika kaunti ya Migori akisema hawezi kuvumilia kuendelea kuishi bila kumwona Bw Raila Odinga akiwa rais wa Kenya.
MWANAUME alijinyonga katika kaunti ya Migori akisema hawezi kuvumilia kuendelea kuishi bila kumwona Bw Raila Odinga akiwa rais wa Kenya.
Mwanaume huyo alichukua hatua hiyo isiyo ya kawaida baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wa Bw Uhuru Kenyatta kuwa rais wa Kenya.
Mkuu wa polisi eneo hilo Bw Richard Bitonga alisema mwanaume huyo alijitia kitanzi nje ya nyumba yake katika kituo cha kibiashara cha Lwanda, eneo bunge la Nyatike.
“Alianza kwa kuvalia jezi la chama cha ODM iliyokuwa na picha ya Waziri Mkuu kabla ya kujitia kitanzi,” akasema Bw Bitonga. Ingawa mwanaume huyo hakuacha ujumbe wowote, alikuwa amewaeleza marafiki wake kwamba alikasirishwa na uamuzi wa mahakama.
Bw Bitonga alisema mwanaume huyo aliye na mke amekuwa mfuasi sugu wa ODM eneo hilo.
Baadhi ya wakazi walisema marehemu alikuwa ametisha kujitoa uhai ikiwa Bw Odinga hangeshinda kesi ya kupinga uchaguzi wa urais. “ Alisema hakuona sababu ya kuendelea kuishi katika ulimwengu huu ikiwa Bw Odinga hatakuwa rais wa nchi hii,” alisema mkazi Bw Samuel Otieno, aliye mchimba dhahabu.
Kusikitisha
Mbunge wa eneo hilo Bw Eric Anyanga alisema kifo cha mwanaume huyo kinasikitisha.
Aliongeza kwamba marehemu alionekana kuvutiwa na sera za Bw Odinga
“Uamuzi wa mahakama ulishtua wafuasi wengi wa Cord kote nchini waliotarajia awamu ya pili ya uchaguzi wa urais baada ya dosari tele kugunduliwa katika uchaguzi wa Machi 4,” alisema Mbunge huyo. Wakati huo huo raia wa Tanzania wanaoishi na kufanya kazi katika mji wa mpakani wa
Isebania wamefuatilia siasa za Kenya kwa karibu katika siku za hivi karibuni huku baadhi yao wakinunua magazeti ya humu nchini kufuatilia matukio ya kumrithi Rais Kibaki.
Baadhi walikusanyika katika makundi wakiwa na marafiki Wakenya kujadili uamuzi wa mahakama ya juu kwa sauti za chini.
No comments:
Post a Comment