More than 40 Gor Mahia fans were robbed of valuables at gunpoint at Kibunja, Molo on Sunday at around 2am. They were on their way to Nairobi from Mumias where they had watched their team lose 2-1 to Western Stima. The highway robbers were dressed in police uniforms.
MASHABIKI WA SIRIKAL WAPORWA NA POLISI BANDIA
Na FRANCIS MUREITHI
Imepakiwa - Monday, May 27 2013 at 15:00
Kwa Mukhtasari
Mashabiki 46 wa klabu ya soka ya Gor Mahia, waliporwa mali yao na majambazi waliokuwa na bunduki wakirejea Nairobi kutoka Mumias Jumapili usiku. Majambazi hao walikuwa wamevalia sare za polisi. Jambo la kuhuzunisha ni kuwa timu yao ilikuwa imecharazwa 2-1 na Western Stima.
ZAIDI ya mashabiki 46 wa klabu ya soka ya Gor Mahia, waliporwa mali yao na majambazi waliokuwa na bunduki wakirejea Nairobi kutoka Mumias Jumapili usiku.
Majambazi hao waliovaa sare rasmi za polisi, waliwavamia kwenye kizuizi bandia cha barabarani eneo la Kibunja, Molo mwendo wa saa nane usiku wakitoka kushangilia timu hiyo ikicheza na Western Stima mjini Mumias.
Dereva wa gari iliyobeba mashabiki wa Gor Mahia, Bw Charles Njuguna, alisema alipofika Kibunja, alisimamishwa na “polisi” kwenye kizuizi cha barabarani na aligundua ni majambazi waliokuwa na silaha walipoingia ndani ya gari aina ya mini-bus.
Alisema mmoja wa majambazi hao alimlazimisha aelekee katika msitu ulio karibu.
“Mmoja wa majambazi alizungumza lugha ya dholuo kwa ufasaha, na kuwaonya abiria washirikiane nao au wauawe mmoja baada ya mwingine,” akasema Bw Njuguna.
Alisema abiria wote waliporwa mali yao ya thamani ikiwemo simu, pesa, viatu na stakabadhi muhimu.
Baadhi ya mashabiki wa Gor Mahia walioandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Molo walisema majambazi hao hawakuwa na haraka na baada ya kupekua gari waliwapora kila kitu mifukoni mwao.
“Hawakuacha chochote hata Sh10 walipotupekua mara ya pili,” akasema shabiki mmoja.
Katika kisa kingine eneo hilo, majambazi hao waliteka nyara matatu ya kampuni ya Molo Line iliyokuwa ikielekea Nakuru kutoka Eldoret na wakamnajisi msichana wa umri wa miaka 20.
Majambazi hao walimlazimisha msichana huyo kutoka ndani ya matatu hiyo iliyokuwa ikielekea Nakuru na kumpeleka kwenye kichaka alipobakwa na wanaume wanane kwa zamu.
Kulala
Alipokuwa akitendewa unyama huo, abiria wengine walikuwa wamelala ndani ya matatu.
Msichana huyo alipelekwa hospitali ya wilaya ya Molo alikotibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Dereva wa matatu hiyo Bw John Kamau alisema alipoteza kila kitu zikiwemo Sh7,000 miongoni mwa stakabadhi zingine muhimu.
Bw Kamau alisema alikuwa na abiria 11 kwenye matatu, na alipofika Kibunja alipata kizuizi cha barabarani na kudhani ni polisi.
Alisema majambazi hao walimvamia alipopunguza mwendo.
“Sikupata kizuizi chochote kutoka Eldoret hadi Molo lakini nilipofika Kibunja nilisimamishwa na watu waliovaa sare kamili za polisi waliokuwa wameweka kizuizi barabarani,” akasema Bw Kamau.
Afisa wa cheo cha juu katika kituo cha polisi cha Molo alisema polisi walianza kuwasaka majambazi hao lakini hadi wakati wa kwenda mitamboni hawakuwa wamemkamata yeyote.
“Tunawaandama majambazi hao lakini kufikia sasa hatujamkamata yeyote,” akasema afisa huyo ambaye hatuwezi kutaja jina lake kwa sababu haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya mkuu wa kituo hicho Bw Job Leskinua.
No comments:
Post a Comment